Niger yaomba msaada wa kuwahudumia wakimbizi
Viongozi wa Niger wametangaza kuwa, nchi hiyo
haina uwezo wa kuwahudumia wakimbizi wanaoingia nchini humo wakitokea katika
nchi jirani ya Nigeria. Maafisa wa serikali ya Niger wanasema, wimbi la
wakimbizi wanaoingia nchini humo limekuwa kubwa mno kiasi cha kushindwa nchi
hiyo kukabiliana nalo. Taarifa zaidi zinasema kuwa, Niger imeiomba jamii ya
kimataifa iisaidie ili iweze kuwahudumia wakimbizi hao. Taarifa ya serikali ya
Niger imebainisha kwamba, inaitaka jamii ya kimataifa iisaidie chakula, ujenzi
wa makazi ya muda na huduma za kitiba na kiafya. Wimbi la wakimbizi wanaoingia
nchini Niger limeifanya nchi hiyo ikabiliwe na hali mbaya zaidi hasa kwa
kuzingatia kwamba, nchi hiyo yenyewe ni miongoni mwa nchi masikini zaidi
duniani na imekuwa ikitaabika kwa ukame na majanga mbalimbali ya kimaumbile.
Wakimbizi hao wamekuwa wakiingia Niger kutokea Nigeria wanakokimbia mashambulio
ya kundi la kigaidi la Boko Haram. Mashambulio ya kundi la Boko Haram la
Nigeria yamepanuka zaidi na kutishia usalama wa raia katika nchi jirani na nchi
hiyo ikiwemo Niger, Cameroon na hata Chad. Nchi jirani na Nigeria tayari
zimeunda kikosi cha pamoja cha kukabiliana na wanamgambo wa Boko Haram.
No comments:
Post a Comment