Zisikupite Stori za MAGAZETI ya leo March 22, 2015,
Nimekupakulia hachini
Hatimaye
mbunge wa Monduli, Edward Lowassa amesema “ameshawishika” na
kuweka bayana kuwa atachukua fomu ya kugombea urais kwa tiketi ya Chama cha
Mapinduzi (CCM).
Lowassa,
ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne, amekuwa akitajwa kuwa
ni mmoja wa makada wa CCM wanaowania urais, lakini hakuwahi kutangaza nia ya
kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini.
Lakini
jana, alilazimika kufunguka kuhusu suala la urais ambalo lilimfanya yeye na
wenzake watano wafungiwe kwa kipindi cha miezi 12 kujihusisha na harakati hizo
baada ya Kamati Kuu ya CCM kuwatia hatiani kuwa walianza kampeni mapema kabla
ya muda kufika.
“Nimepata barua za ushawishi kutoka kwa watu wengi, lakini
nyinyi nimeshawishika,” alisema Lowassa nyumbani kwake mjini Dodoma
wakati alipokuwa anazungumza na masheikh wa misikiti ya Wilaya ya Bagamoyo
wanaokadiriwa kuwa kama 50 hivi ambao pia walikuja mjini hapa kwa ajili ya
kumshawishi aingie kwenye kinyang’anyiro cha urais na kumkabidhi mchango wa
Sh700,000 za kuchukulia fomu.
“Lakini bado kuna taratibu za chama za kuheshimu. Nangojea
pale watakaposema sasa tuwe, basi itakuwa.”
Lowassa
alifungiwa na CCM Februari 18, 2014 pamoja na Bernard Membe, ambaye ni
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Steven Wasira (Kilimo, Chakula na Ushirika), na January Makamba
(Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).
Wengine
waliofungiwa ni Frederick Sumaye, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali
ya Awamu ya Tatu na William Ngeleja (Mbunge wa Sengerema).
Pamoja
na adhabu hiyo kumalizika Februari 18, CCM imesema Kamati ya Maadili inaendelea
na uchunguzi kwa ajili ya kujiridhisha kama miongoni mwao kuna waliokiuka
adhabu hiyo kabla ya kuwasilisha mapendekezo kwenye Kamati Kuu ambayo itafanya
uamuzi.
Masheikh
waliofika jana nyumbani kwake wanatoka maeneo ya Mlingotini, Kondo, Kaole,
mjini Bagamoyo, Lugoba na Chalinze wilayani Bagamoyo.
Mbali
na kumuomba atangaze nia, masheikh hao pia walimsomea dua ya kumtakia heri
katika harakati hizo.
“Nyie ni special (maalum), mnatoka Bagamoyo na inajulikana kwa
historia na ni nyumbani kwa Rais (Jakaya Kikwete). Namimi nimepata baraka zake
na nyie mmemuwakilisha,”Lowassa.
“Tumetoka naye mbali sana, lakini Mwenyezi Mungu akinijalia
nitaanzia pale alikomalizia. Amefanya kazi kubwa na ya heshima kwa kweli. Kwa
hiyo kitendo cha kutoka nyumbani kwenu kuja kuniona kwa kweli kimenipa nguvu
kwamba wenzangu wa Bagamoyo wako pamoja na mimi.”
MWANANCHI
Ikiwa
ni siku moja tangu Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kutangaza
kung’atuka katika nafasi yake ya ubunge, Bunge limeeleza kuwa mbunge huyo
atapata mafao yake yote kama wabunge wengine.
Zitto
ambaye alitangaza juzi bungeni kuwa anaondoka baada ya kuvuliwa unanachama wa
Chadema aliahidi kuwa ‘Mungu akipenda’ atakuwa tena ndani ya chombo
hicho cha kutunga sheria Novemba mwaka huu baada ya uchaguzi mkuu.
Kuondoka
kwa mbunge huyo pia kunaifanya nafasi ya uenyekiti wa Kamati ya Hesabu za
Serikali(PAC) kuwa wazi kwa kuwa ndiye aliyekuwa akiishikilia hadi alipotangaza
rasmi juzi kuachia ubunge.
Akizungumzia
uamuzi wa Zitto na juu ya mafao yake baada ya kuamua kuondoka mwenyewe,
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema kuwa mbunge huyo
atalipwa mafao yake yote.
“Unajua Chadema wametangaza kumvua uanachama Zitto lakini
hawajampa barua, sasa yeye ameona kuwa kuliko kuendelea na ubunge wake ni vyema
akakaa kando. Kutokana na suala hilo atalipwa tu mafao yake yote,” Joel.
Katika
hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wa PAC wamesikitishwa na kuondoka kwa Zitto
kabla ya muda wa Bunge la 10 kumalizika huku wakimwelezea ni kiongozi aliyeweza
kuwaunganisha katika kamati bila kujali itikadi za vyama.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti jana, wajumbe hao walisema aliwafanya wajumbe wa kamati
hiyo kuwa familia na aliwaamini na kuwaheshimu wote.
“Ni mtu aliyekuwa na ushirikiano na aliweza kutuunganisha bila
kujali itikadi.
“Alitufanya kama familia na alituamini na kutuheshimu. Tunamtakia
kila la kheri katika mipango yake ijayo,”Ismail
Aden Rage .
MWANANCHI
Waziri
wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira aliyepewa jukumu la
kuandaa Ilani ya CCM kwa ushirikiano na timu ya watu 23 wa chama hicho
itakayotumia kwenye kampeni za uchaguzi wa mwaka 2015 hadi 2020, amejitokeza na
kusema kazi hiyo ipo ukingoni kukamilika.
Kauli
hiyo Wasira ameitoka siku moja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye kuwaeleza waandishi wa habari mjini Arusha kuwa Ilani hiyo
inasimamiwa na Wasira na inatarajia kutoa Dira ya Mwelekeo ya chama hicho
tawala katika kutatua matatizo ya wananchi.
Alisema
Ilani hiyo itaangazia pia mambo ambayo yaliahidiwa ndani ya Ilani iliyopita na
hayakutekelezwa ipasavyo. Baadhi ya mambo ambayo hayakufanikiwa ni tatizo la
maji, migogoro ya ardhi na suala la ajira.
Akizungumza
jana na gazeti hili kwa njia ya simu, Wasira alisema: “Unajua labda ninyi mtakuwa mmechelewa kupata taarifa kuwa
tumeanza lini, lakini sisi tulikwishaanza kazi hii na tuko hatua za mwisho za
kutoa Rasimu ya Ilani yenyewe.”
Wasira
ambaye pia ni Mbunge wa Bunda alisema Ilani hiyo inaandaliwa kwa kuangalia
changamoto gani zilizojitokeza kwa miaka 10 nyuma na ndiyo wanayoipa kipaumbele
katika maandalizi hayo.
“Ukiangalia uchumi umekuwa ukikua kwa asilimia saba kila mwaka
lakini si kiwango kikubwa ukilinganisha na maisha ya wananchi yalivyo hivyo
Ilani hii itatakiwa kuja na majibu ya tatizo hilo na kuhakikisha wananchi wetu
wanakuwa na maisha bora,” Wasira.
“Suala la ajira ukiangalia wanafunzi wengi wanaanza shule za
msingi na wanapomaliza wanaendelea sekondari na baada ya hapo wanakwenda vyuoni
hivyo wahitimu wa vyuo vyetu wanaongezeka jambo hapa ni kuja na mkakati wa
kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wetu.”
HABARILEO
Mitambo
ya kufua umeme inayotumia mafuta kwa ajili ya kufua umeme nchini, imetajwa kuwa
kikwazo katika maendeleo ya Taifa, kutokana na kutumia rasilimali fedha za
kigeni nyingi katika kuzalisha nishati hiyo nchini, ambayo ingeweza kutumika
katika maendeleo.
Taarifa
za uhakika kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme (Tanesco),
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
na Benki Kuu (BoT), zimebainisha kuwa
suluhisho pekee la tatizo hilo, ni kukamilika na kuanza kazi kwa bomba la gesi
kutoka Madimba Mtwara, hadi Kinyerezi, Dar es Salaam.
Trilioni
1.6 Taarifa ya TPDC kwa umma iliyotolewa mwishoni mwa wiki kuhusu utekelezaji
wa ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia kutoka Madimba, Mtwara hadi Kinyerezi
Dar es Salaam, imeeleza kuwa ununuzi wa mafuta hayo ya kufua umeme umekuwa
ukigharimu Taifa zaidi ya Sh trilioni 1.6 kila mwaka.
“Itakapokamilika miundombinu hiyo (ujenzi wa bomba la gesi), itaokoa
zaidi ya Dola za Marekani bilioni moja sawa na Sh trilioni 1.6 kwa mwaka,
zinazotumika kwa sasa kuagiza mafuta kwa ajili ya kufua umeme kwa kutumia
mitambo ambayo tayari ipo nchini,”
imeeleza taarifa hiyo.
Mitambo
hiyo ni pamoja na mtambo wa IPTL uliopo Tegeta Dar es Salaam unaotumia mafuta
mazito na mitambo ya Agreko na Symbion iliyopo Dar es Salaam, inayotumia gesi
inayoagizwa kutoka nje.
Mwingine
ni mtambo wa Symbion wa Dar es Salaam pia, ambao unatumia mafuta ya kurushia
ndege na mitambo mingine miwili ya Symbion ya Dodoma na Arusha, ambayo inatumia
gesi inayoagizwa kutoka nje.
Tanesco
inavyonyonywa Taarifa kutoka Tanesco zimebainisha kuwa kitendo cha mitambo hiyo
kutumia mafuta mazito, mafuta ya ndege na gesi kutoka nje ya nchi, badala ya
gesi asilia kufua umeme, kimekuwa ‘kikitafuna’ shirika hilo, kwa kuwa wamiliki
wa mitambo hiyo huuza umeme kwa shirika hilo kwa bei ya juu, kuliko bei ambayo
Tanesco inalazimika kuuza kwa wananchi.
HABARILEO
Shamba
la miwa inayokadiriwa kufikia tani 6,000 baada ya kuvunwa lenye ukubwa wa hekta
240, limechomwa moto na watu wasiojulikana na kusababisha hasara ya Sh milioni
280.2, mali ya wakulima wa wilaya ya Missenyi mkoani Kagera.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti juzi, wakulima hao walisema kuwa vitendo hivyo vya jamii
kuendelea kuchoma moto hovyo nyikani vimeanza kurejea.
Mmoja
wa wakulima hao, Anas Swaibu alisema uchomaji moto hovyo umekuwa
changamoto kuu inayorudisha nyuma maendeleo ya mkulima na kumsababishia
kutotimiza malengo yake.
Alisema
kuwa athari ya moto mashambani, imekuwa ikisababisha mkulima kulazimika kuvuna
miwa yake kabla haijakomaa, huku uamuzi huo ukimuingiza hasara kwani malengo ya
mavuno yake hushindwa kukamilika ipasavyo.
Kutokana
na athari zinazoendelea kusababishwa na vitendo vya uchomaji moto hovyo,
mkulima huyo ameuomba uongozi wa serikali ya wilaya kuangalia upya jinsi gani
utawala utaweza kushirikisha jamii katika kutokomeza majanga hayo.
“Tunaomba Serikali ifanye utaratibu wa kukutanisha wadau wa
maendeleo, wakulima na jamii kwa ujumla ili kuangalia ni jinsi gani tunaweza
kutokomeza vitendo hivi kwani kila siku mkulima anazidi kuumia jambo ambalo
linarudisha nyuma maendeleo yake,”alisisitiza.
Alisema
kuwa kwa sasa bei inayotolewa na mnunuzi mkuu ambaye ni kiwanda cha Sukari cha
Kagera kilichopo wilayani humo ambayo ni Sh 46,700 kwa tani moja, kiasi ambacho
kiko chini na hakiendani na gharama za uzalishaji katika kilimo hicho.
Alisema
shughuli za kilimo cha miwa zinachukua gharama nyingi ukilinganisha na bei
inayotolewa kiwandani, japo angalau bei inapaswa kufikia kiasi cha Sh 55,000
kwa tani ili mkulima aweze kupata faida na kukidhi mahitaji yake ya msingi
ukilingaisha na gharama za kilimo kupanda.
“Mitaji ya wakulima ni mikopo, hivyo tunalilia bei kwa mnunuzi
tukiwa na maana ya kwamba tuweze kurudisha mikopo ya benki na sisi tunufaike na
kilimo hiki, kuliko kushindwa kurudisha hata mikopo na kufilisiwa na
waliotukopa,” alisema.
Hata
hivyo, licha ya kutoridhika na bei hiyo inayotolewa na mnunuzi wa kiwanda
hicho, mkulima huyo ametoa shukrani kwa uongozi wa kiwanda cha Sukari Kagera
Sugar kwa kutoa msaada mkubwa kwa wakulima vinginevyo kama uongozi usingekuwa
karibu na wakulima hao, hakuna ambaye angelikuwa anaendelea na shughuli za
kilimo hadi sasa.
MTANZANIA
Rais
wa zamani wa Malawi Joyce Banda amekimbilia nchini Marekani kuomba
hifadhi ya kisiasa.
Chanzo
cha kuaminika kutoka Marekani kilisema Banda ameshapewa hifadhi na Serikali ya
Marekani ingawa inafanywa kwa siri.
Banda
akiwa nchini humo amekuwa akishiriki hafla mbalimbali anazoalikwa na moja ya
hafla aliyoalikwa ni ile ya utoaji tuzo ya kimataifa ya uongozi ya taasisi ya
GB Group Global ya Marekani ya mwaka 2015 iliyofanyika katika jiji la
Washington.
“Ni kweli Joyce Banda yupo nchini Marekani kwa muda mrefu
sasa,na katika hafla hiyo alisema alipokuwa rais kwa muda mchache alijenga wodi
za wazazi zilizowasaidia wanawake nchini Malawi kujifungua katika mahali salama”
kilisema chanzo hicho.
Chanzo
kingine kilisema Juni mwaka jana baada ya Peter Mutharika kuapishwa kuwa
rais mpya wa Malawi ndipo Banda alipokimbilia Marekani.
JAMBOLEO
CHADEMA
imesema aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe angerithi
mikoba ya Mwenyekiti wake Freeman Mbowe au Dk. Slaa kama angekuwa
na nidhamu na kutokuwa msaliti.
Pia
kimesema hakitamsahau Zitto kwa kwani alikuwa na mchango mkubwa ndani ya chama
hicho.
Mnadhimu
mkuu wa kambi ya upinzani Tundu Lissu alisema Zitto alikuwa na mazuri
yake ndani ya chama hicho na ni miongoni mwa watu waliokuwa wakipewa nafasi
kubwa ya kurithi mikoba ya viongozi wetu wa ngazi ya juu.
Pia
Lissu alifafanua kuwa aliamua kutompa Ziito mkono wa kumuaga baada ya kutangaza
uamuzi huo bungeni kwa kuwa kufanya hivyo kungemfanya aonekane mnafiki.
Amesema
anasimamia anachokiamini kuhusu kasoro alizozifanya Zitto za kumfanya atimuliwe
na aliamua kuondoka kwa kuwa alijua kinachofuata kwa kuwa alikiuka katiba ya
chama inayokataza mambo ya chama kupelekwa mahakamani.
NIPASHE
Polisi
Jijini Arusha wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananachi
wenye hasira waliochoma nyumba na magari baada ya kijana wao anayetuhumiwa
kufumaniwa akifanya mapenzi na mfanyakazi wa ndani kuuawa na anayedaiwa kuwa
bosi wa mfanyakazi huyo.
Bosi
huyo mkazi wa mtaa wa Olasiti Arusha pamoja na wenzake wawili wanatuhumiwa
kumuua kijana huyo Melita Mokosio baada ya kumfumaini akifanya ngono na
msichana huyo hatua iliyosababisha wakazi wenye hasira kuchoma nyumba yake na
magari matatu ya waliohusika na mauaji hayo.
Watu
walioshuhudia tukio hilo lililotokea majira ya saa3 asubuhi walimtaja
anayedaiwa kumuua kijana huyo ambaye anajulikana kwa jina la baba Tony.
Kaimu
kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha Edward Balele aliyekuwa eneo la tukio
alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na uharibifu wa mali lakini alisema jeshi
lake linafanya uchunguzi wa tukio hilo kabla ya kutoa taarifa rasmi.