WAZAZI WASHINDWA KUDHIBITI MATUMIZI YA MITANDAO KWA WATOTO WAO.
Hamjambo nduguzangu, na karibuni kujiunga nami katika makala
hii ambayo huangazia taathira za teknolojia mpya za mawasiliano na
habari hasa intaneti katika mtindo wa maisha ya mwanadamu. Katika muundo
wa vyombo vya habari duniani bado tunashuhudia uwajibikaji. Hii ndio
sababu kuna televisheni au mashirika ya filamu ambayo hutangaza wazi
kuwa baadhi ya filamu au vipindi vitazamwe tu na watu wa umri maalumu.
Lakini baada ya kuibuka intaneti na kuenea idadi ya watumizi wake
miongoni mwa watu wote katika jamii kumejitokeza hatari kubwa.
Tunakumbusha hapa kuwa kama ambavyo intaneti ina faida kubwa sana pia
inaweza kuwa chanzo cha matatizo na hatari kubwa haswa kwa watoto.
Kwa
mujibu wa takwimu zilizopo, idadi kubwa ya wazazi hawadhibiti namna
watoto wao wanaovyotumia intaneti na wala hawalipi uzito suala hilo.
Hata baadhi ya wazazi hawajui namna ya kutumia intaneti ili waweze
kudhibiti na kusimamia utumizi wake miongoni mwa watoto wao. Kwa hivyo
kuna haja kubwa kwa wazazi kujifunza matumizi ya intaneti ili waweze
kudhibiti na kusimamia namna watoto wao wanavyotumia teknolojia hii mpya
na ya kisasa. Kutokana na kuwa kizazi cha teknolojia hubadilika
sambamba na kubadilika kizazi cha wanaadamu, kwa ujumla wale wenye umri
wa juu huwa wavivu au wasio kuwa na hamu ya kukumbatia kizazi kipya cha
teknolojia. Natija ya awali ya mgongano huu ni kuibuka ufa mkubwa baina
ya vizazi sambamba na kutofautiana kuhusu namna ya kutumia teknolojia ya
mawasiliano. Hatimaye huwa tunashuhudia mtoto akichukua mahala pa mzazi
au mwanafunzi mahala pa mwalimu katika kutoa mafunzo kuhusu utumizi wa
teknolojia mpya. Kutokana na kuwa wazazi wengi wana ujuzi wa chini
katika masuala ya teknolojia ikilinganishwa na watoto wao, wakati
mwinginine hushuhudiwa kutokuwepo na heshima ya kutosha katika uhusiano
wa mzazi na mtoto. Kwa msingi huo kuna haja ya watoto kuzingatia maadili
ya kijamii na kuwapa wazazi heshima wanayostahiki ili msingi wa familia
uweze kudumishwa.
Aghalabu ya watoto hasa wenye umri wa chini
huitazama intaneti kama chombo cha kujifurahisha na kuchezea. Kwa hivyo
watoto wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi kwani hawajui ni jambo gani
wanalotaka na kulitafuta. Moja ya nuksani kubwa ya intaneti ni kuwa
inatoa maudhui mbaya na nzuri papo hapo.
Kutokana na kuenea intaneti
ndani ya nyumba ima kupitia kompyuta za kawaida au simu za mkononi
tumeshuhudia namna malezi ya kiintaneti yanavyochukua nafasi ya malezi
ya kifamilia. Tunashuhudia kustawi kwa kasi teknolojia ya habari na
mawasiliano na hivyo mtoto wa sasa anaweza kutumia intaneti kujua
takribani kila kitu pasina kuwepo mipaka. Hivi sasa fmailia nyingi hasa
katika nchi zilizostawi haziwezi kuwazuia watoto wao kutumia teknolojia
za kisasa kama vile intaneti na hivyo ile mipaka ya kuta nne za nyumba
haiko tena. Kuna natija mbili kuhusu utumizi wa intaneti miongoni mwa
watoto, awali ni kuwa iwapo wataitumia teknoljia hii kwa njia sahihi
basi wataweza kufaidika sana hasa kielimu na katika upande wa pili iwapo
teknolojia hii itatumika vibaya ndani ya nyumba si tu kuwa watoto
watafeli katika masomo yao bali pia watakuwa na maadili maovu na pia
kuharibu uhusiano na wazazi wao.
Wataalamu wa saikolojia wanaamini
kuwa watoto wengi wanaelekea katika intaneti kutokana na mvuto wake,
kujaza wakati wao wa mapumziko, kujaza pengo la nuksani katika maisha
yao, kukosa utambulisho sahihi na pia kutokana na kuvurigika uhusiano
baina yao na wazazi.
Wataalamu wa masuala ya jamii wanaamini kuwa,
kuenea teknolojia ya habari na mawasiliano ni chanzo cha matatizo na
upotofu wa kiutamaduni na kijamii duniani. Kuingia teknolojia ya
mawasiliano manyumbani kuna maana ya kuingia kitu kipya na
kisichojulikana ndani ya nyumba!
Iwapo teknolojia hii itatumiwa
vibaya, basi kutatoweka fursa ya maingiliano ya kawaida baina ya jamaa
katika familia na jambo hilo huibua hali ya kujitenga, upweke na
ubinafsi miongoni mwa watu wanaoishi chini ya paa moja. Aidha intaneti
huwafanya baadhi ya watu hasa watoto na mabarobaro kuwa ni wapokezi wa
kilicho mbele yao pasina kuwa na uwezo wa kutosha wa kuchagua, kuchambua
na kutafakari. Pamoja na hayo yote, tutake tusitake teknolojia sasa ni
sehemu isiyotenganika na maisha ya kisasa. Leo watoto kuanzia umri wa
hata chini ya miaka mitano wana hamu ya kuingia kwenye intaneti. Kwa
hivyo sambamba na faida za teknolojia, hii kuna matatizo mengi ambayo
huwakumba watu dhaifu kifikra katika jamii.
Leo wazazi na watoto
hutumia wakati wao mwingi katika teknolojia za kidijitali ikiwemo
intaneti na televisheni na hivyo hakupatikani fursa ya kutosha ya wazazi
kuzungumza kwa karibu na watoto wao. Intaneti na vyombo vya habari vya
kidijitali hupelekea kuongozeka ubinafsi na kujitenga mtu na jamii na
hivyo kuporomoka zile thamani za maingiliano ya kijamii. Hivi sasa
mabarobaro na vijana wengi wanatumia teknolojia mpya za habari na
mawasiliano kupata elimu na maarifa. Hata watoto wadogo sawa na
mabarobaro nao pia wanatumia teknolojia mpya kujitambulisha kuwa na
marafiki kusoma na kuwasiliana na jamaa na marafiki. Kwa hivyo intaneti
imegeuka na kuwa mwalimu katika maisha ya watoto na kwa kutegemea jinsi
inavyotumika inaweza kuwa mwalimu mbaya au mzuri. Tatizo hili litakuwa
sugu zaidi katika siku za usoni baada ya kuanza kutumika kizazi kipya
cha intaneti iliyopewa jina la Web 4 ambayo haitawezekana kuifanyia
filtering au kuzuia baadhi ya kurasa au tovuti za intaneti. Kwa mujibu
wa inteneti hiyo ya mustakabali usio mbali wazazi na hata serikali
haitaweza kudhibiti moja kwa moja kurasa zinazotembelewa hasa na watoto.
Kwa msingi huo malezi yanatazamiwa kuondoka katika mkondo huu wa sasa
na kuelekea upande wa kujilea au kujielimisa kupitia intaneti. Hapo
hatari kubwa ni kuwa watoto wadogo, mabarobaro na vijana watakumbana na
thamani nzuri na mbaya kwa pamoja na iwapo hakutakuwepo na muongozo
sahihi basi wengine wataporomoka kimaadili na hali hiyo kuenea katika
jamii.
Kwa hivyo kuna haja kwa wazazi kupata mafunzo kamili na ya
kina kuhusu utumizi wa intaneti na teknolojia husika ili waweze kuwapa
watoto ushauri na muongozo sahihi. Kinyume na hili hawatakuwa na uwezo
wa kutoa ushauri kwa watoto wao. Wazazi wanapaswa kufahamu kuwa
teknolojia ya habari na mawasiliano na hasa intaneti ni zaidi ya chombo
cha kujipatia maarifa na kucheza. Kwa hakika intaneti sasa ni chombo
kinachoweza kujenga au kusambaratisha utamaduni asili kwa hivyo kuna
haja kwa walimu na wazazi kuinua kiwango chao cha ufahamu na ujuzi wa
teknolojia za kisasa zinazotumiwa na watoto. Kwa mfano katika baadhi ya
nchi hasa za Magharibi imebainika kuwa watoto walio kati ya umri wa
miaka hadi minane hufuatilia kazi ambazo huwa wamekatazwa. Wakiwa kwenye
intaneti huenda katika tovuti au mitandao ya kijamii wanakoweza kujuana
na watu ambao ni hatari. Katika umri huu wazazi wanapaswa kuwaongoza
watoto wao watembelee tovuti ambazo ni maalumu kwa watoto ili
wasihadaiwe na watu wanaotaka kuwadhalilisha kijinsia. Watoto walio na
umri wa kati ya miaka 9 hadi 12 huwa wameshaanza kutambua tafauti za
kijinsia baina ya mwanaume na mwanamke na hivyo wazazi hapa pia
wanapaswa kuchukua tahadhari ili watoto wao wasije wakatumbukia katika
tovuti za ufuska
No comments:
Post a Comment